JINSI YA KUPANGA BAJETI YA MSHAHARA WA KWANZA
UTANGULIZI
Kupanga bajeti ni kitu cha msingi sana hasa kwa mshahara wa kwanza kwasababu kiuhalisia mshahara wa kwanza ndio huwaumiza watu wengi sana hushangaa umeisha vipi na kuanza kusema kuwa hautoshi kumbe tatizo lipo kwenye kutopanga bajeti ya mshahara kabla haujaingia
Umeanza kazi, mshahara umeingia kwenye akaunti yako Tsh 600,000.
Siku mbili tu Tsh 450,000 zimeshaisha. Unajiuliza pesa yangu imeenda wapi?
Usiwe na wasiwasi sote tumepitia hapo. Mshahara wa kwanza bila mpango ni kama maji kwenye kikapu.
Leo nakupa hatua 5 rahisi utakazotumia leo hii ili mshahara wako udumu hadi mwezi ujao. Hii ndio "Pesa Hatua kwa Hatua" halisi.
Hatua ya 1: Toa 10% Kwanza Kabla ya Kitu Kingine
Hii ndio sheria namba 1, Pesa ikiingia, kabla hata hujalipa kodi ya nyumba, toa 10%. Hii ni kwaajili ya kiweka akiba
Kama mshahara wako ni Tsh 600,000, toa Tsh 60,000 weka pembeni. Sehemu ya kuiweka unaweza kufungua akaunti nyingine tofauti au tumia M-Pesa wallet tofauti. Usiiweke na pesa ya matumizi, ukichanganya utaitumia tu.
Kumbuka, hii sio iliyobaki hii ni ya kwanza. Lipia mustakabali wako kwanza.
Hatua ya 2: Gawa masanduku 4 makubwa
Sahau kutumia ovyo, gawa pesa yako kwenye masanduku 4. Tumia karatasi au notes ya simu.
1. Nyumba na Chakula: 50%
Hapa ndio Tsh 300,000. Kodi, umeme, maji, chakula cha mwezi mzima. Hapa itaigawa vizuri kwapangilio mfano kodi Tsh 100,000, umeme na maji 20,000, chakula 180,000.
2. Usafiri na mawasiliano: 15%
Tsh 90,000, hii ni kwaajili ya bando daladala, weka bajeti ya wiki 22,500, ikiisha unangoja wiki ijayo.
3. Madeni: 5%
Tsh 30,000. Hapa ndio utalipa deni kama una au kuongeza akiba yako.
4. Matumizi binafsi na burudani: 10%
Tsh 60,000, hii ni yako, Nenda kula chips, nunua nguo. Lakini ukiimaliza, imeisha usitoe kwenye sanduku lingine.
5. Dharura na msaada: 10%
Tsh 60,000, hii ni kwaajili ya dharura ikitokea, ni muhimu sana kwasababu dharau hutokea sana katika maisha ya kila siku, pia kusaidia watu wenye uhitaji. Sanduku hilo litafanya kazi hizo.
Hatua ya 3: Andika Kila Tsh 1000 inakotoka
Watu wengi wanapoteza pesa kwa vitu vidogo vidogo.
Kuanzia leo, kwa siku 30 zijazo andika kila unachotumia, unanunua soda Tsh 1000 andika, unapanda boda Tsh 2000 andika. Hii itakusaidia kufahamu matumizi makubwa yanatoka kwenye kitu gani. Mwishoni mwa wiki utashangaa. Aisee nimespend Tsh 40,000 kwenye soda tu?, ukiiona ndio utaweza kuikata. App rahisi ya kutumia ni Money Manager au tumia tu daftari.
Hatua ya 4: Epuka marafiki wa Mshahara
Siku 3 mshahara ukiingia, simu yako itaanza kuita, mkuu nisaidie kidogo, tunapiga story leo. Sio mbaya kusaidia, lakini weka sheria. Weka Tsh 20,000 kwenye sanduku la msaada. Ikiisha, jibu mwezi ujao, ndugu kama utampa kila mtu, mwezi utamaliza na deni.
Hatua ya 5: Panga Kabla ya tarehe 25
Usisubiri mshahara uingie ndio upange. Tarehe 25, kaa chini dakika 20, Angalia bajeti ya mwezi ujao. Kodi ni kiasi gani? Chakula? Kuna harusi?. Ukipanga mapema, unakuja na utulivu, huwezi kushangazwa.
HITIMISHO
Mshahara sio tatizo, tatizo ni mpango, Tsh 600,000 zinaweza kutosha, Tsh 2,000,000 pia zinaweza zisiweze, Tofauti ni mpango.
Anza na hatua 2 leo: Toa 10% na andika matumizi yako. Mshahara wako wa kwanza usiwe wa mwisho kujipanga.
Wewe unasikiaje? Ni kosa gani kubwa ulilifanya mshahara wako wa kwanza? niandikie kwenye comment hapo 👇
Maoni
Chapisha Maoni