JINSI YA KUJENGA AKIBA YA DHARURA HATA KAMA KIPATO NI KIDOGO
UTANGULIZI
Akiba ya dharura ni moja ya kinga muhimu zaidi katika maisha ya fedha. Hii ni pesa inayokusaidia wakati mambo yasiyotarajiwa yanapotokea, kama ugonjwa, kupoteza kazi, au gharama za ghafla nyumbani.
Watu wengi hudhani lazima uwe na kipato kikubwa ili kuanza akiba ya dharura. Hilo si kweli, kitu muhimu ni kuanza na kiasi kidogo unachoweza kumudu, unaweza kuanza kwa kuweka pembeni kiasi fulani kila wiki au kila mwezi bila kusubiri mpaka upate pesa nyingi. Unaweza kuanza akiba ya dharura hata kwa Tsh 1000 leo hii.
![]() |
Lengo la makala hii ni kukupa hatua 6 za vitendo, bila nadharia nyingi, za kujenga akiba hata kama unapata Tsh 200,000 - Tsh 500,000 kwa mwezi.
Hatua ya 1: Anza na lengo la Tsh 50,000
Usianze na milioni, ubongo utakukataa. Lengo la kwanza: Fika Tsh 50,000. Hii inaweza kulipia usafiri kwenda hospitali, dawa, au chakula cha wiki 1. Ukishafika 50k, utapata morali ya kwenda 100k, 200k...
Hatua 2: Tumia kanuni ya 10% au 5%
Kila ukipata pesa, toa asilimia kwanza kabla ya matumizi mengine. Mshahara Tsh 300,000 x 10% = Tsh 30,000 kwa mwezi au mshahara Tsh 200,000 x 5% = Tsh 10,000 kwa mwezi.
Hii ndio siri ya watu waliopata mali, lipa wewe mwenyewe kwanza.
Hatua ya 3: Tenga akiba na matumizi
Usiiweke kwenye M-Pesa yako ya kawaida. Utaitumia.
Fanya moja ya hizi:
1. M-Pesa/Tigo Pesa Lock - Inakufungia pesa miezi 3
2. Akaunti ya Benki tofauti - CRDB, NMB. Usibebe ATM yake
3. Nguruwe ya nyumbani - Ya zamani lakini inafanya kazi
4. SACCOS
Hatua ya 4: Pata Tsh 20,000 ya ziada kila wiki
Hata na kipato kidogo unaweza:
1. Uza nguo zako za zamani Facebook Marketplace
2. Fanya Delivery weekend
3. Pika chipsi uuze ofisini
4. Fundisha mtoto masomo Tsh 10,000 kwa wiki
Hii Tsh 20,000 x wiki 4 = Tsh 80,000 kwa mwezi kwenye akiba yako.
Hatua ya 5: Jenga tabia sio kiasi
Ni bora uweke Tsh 2000 kila wiki kwa mwaka mzima, kuliko kuweka Tsh 100,000 mwezi 1 halafu uache.
Tabia ndio inayojenga utajiri, Kiasi kinakuja baadaye.
Hatua ya 6: Weka sheria ya sitatumia akiba hii kwa matumizi mengine tofauti na dharura
Andika kwenye karatasi na ubandike ukutani: NITATUMIA AKIBA HII IKIWA TU: 1. Hospitali 2. Kufukuzwa 3. Ajali
Kila ukitaka kuitumia kununua simu, soma hiyo karatasi kwanza.
MAKOSA 4 YA KUEPUKA
1. Kukopa ukiwa na akiba - Kama una Tsh 100,000 akiba na unataka kununua TV, subiri. Usikope.
2. Kutumia akiba kwa dharura za uongo - harusi ya ndugu sio dharura.
3. Kutokurudisha - ukitumia Tsh 50,000 kwa dharura, panga jinsi ya kuirudisha ndani ya miezi 3.
4. Kulinganisha na wengine - rafiki yako ana 2 milioni. Wewe anza na 10,000 zako.
HITIMISHO
Njia bora ni kuweka lengo maalum. Kwa mfano, unaweza kuamua kujenga akiba ya miezi miwili au mitatu ya matumizi yako muhimu. Ukishakuwa na lengo, inakuwa rahisi kufuatilia maendeleo yako.
Ni vizuri akiba hii ikawekwa sehemu iliyo salama na rahisi kufikiwa, lakini si sehemu ambayo utaitumia kwa urahisi kwa mambo yasiyo ya dharura. Kumbuka, akiba ya dharura si pesa ya sherehe wala safari za ghafla. Ni kinga ya utulivu wako wa kifedha. Ukiwa nayo, changamoto za maisha hazitakusukuma kila mara kuomba msaada au kuingia kwenye maden
Usisubiri kuwa na pesa nyingi ili uanze kuweka akiba. Anza kuweka akiba ndipo utakuwa na pesa nyingi. Fikiria hivi: baada ya miezi 12, utapenda kuwa na Tsh 0 au kuwa na Tsh 240,000? Chaguo ni lako. Na linaanza na Tsh 1000 leo.
Leo utaanza na Tsh ngapi? Andika comment chini Naanza na Tsh tujipe moyo wenzetu 👇
Ukipenda makala kama hizi za Pesa Hatua kwa Hatua, share na rafiki 1 anayehitaji kuisoma.

Maoni
Chapisha Maoni