TABIA ZA KILA SIKU ZINAZOHARIBU MPANGO WAKO WA FEDHA BILA KUJUA
Je unafahamu mpango wako wa kifedha unaharibiwa na vitu gani?
Mara nyingi, si maamuzi makubwa tu yanayouvuruga mpango wa kifedha, bali tabia ndogo za kila siku zinazoonekana ndogo lakini zikiungana zinakula kipato chako kwa kiasi kikubwa. Makala hii inaonesha tabia baadhi na jinsi ya kuanza kuzibadilisha au kuziacha.
Tabia ya 1: Kutoandika matumizi yako ya kila siku
Kitendo cha kutokujua pesa zinaishia wapi mara nyingi kunatokana na kutokuandika matumizi yako ya kila siku. Mfano; matumizi ya chakula, usafiri, vocha, na mambo mengine. Usipoandika utatumia pesa bila mpangilio maalumu na utashangaa pesa zinaisha kabla ya siku ulizopanga au matumizi yanakuwa nje ya mpango uliojiwekea. Hivyo kutoandika matumizi yako ni tabia inayoharibu mpango wako wa kifedha taratibu bila kujua na hatimaye utakusababishia kutokuwa na uhuru wa kifedha
Suluhisho: Ili uweze kurekodi matumizi yako tumia daftari dogo au app rahisi kama app ya notes kuandika kila matumizi yako ya kila siku hata kama ni kidogo sana, hii itakusaidia kutambua mwelekeo wa matumizi yako, na kuwa mwaminifu katika kuitekeleza mipango ya kifedha unayojiwekea.
Tabia ya 2: Matumizi nje ya bajeti au ununuzi wa vitu kwa haraka bila mpango (impulse buying)
Kununua vitu kwa sababu tu umeviona, si kwa sababu vilikuwa kwenye mpango, ni chanzo kikubwa cha matumizi yasiyodhibitika. Watu wengi sana wanaanguka katika tabia hii kwasababu wanafanya maamuzi kwa hisia na kusahau kuwa wanafanya kitu ambacho hakikuwa katika mpango au hakikuwa ndani ya bajeti, hii huchochea sana kuharibika kwa mpango wako wa kifedha.
Suluhisho: Ili kuondokana na tabia hii ya kuwa na matumizi nje ya bajeti, tengeneza orodha ya ununuzi kabla ya kwenda dukani na ushikilie orodha hiyo au weka mpango wa kununua kitu fulani kwa wiki hii na kingine inayofuata hii itasaidia sana kutokuwa na matumizi nje ya bajeti yako, na mpango wako wa kifedha kwenda sawasawa na ulivopanga.
Tabia ya 3: Kutumia mikopo kuficha pengo la bajeti kila mwezi
Pia hii ni tabia inayoharibu mpango wako wa kifedha taratibu badala ya kurekebisha bajeti kama kupunguza matumizi,kutumia mikopo kama plasta kila mwezi kunazidisha tatizo kwasababu mikopo hurudishwa kwa riba na ndio huongeza deni kuwa kubwa zaidi. Hivyo hutakiwi kutumia mkopo ili tu kuficha pengo la bajeti yako ya kila mwezi hii ndio hatari zaidi kwasababu mwisho wa siku utashindwa kulipa deni kwa wakati na litaendelea kuongezeka, mpango wako wa kifedha utaharibika vibaya na utakosa kuwa na uhuru wa kifedha.
Suluhisho: Ili kuithibiti tabia hii weka lengo la mwezi mmoja bila kukopa, hata kama inamaanisha kupunguza kiwango cha starehe.
Tabia ya 4: Kutojipangia kiasi cha akiba
Tabia ya kutopanga kiasi cha kuweka akiba, mfano leo umeweka asilimia 10 kesho 20, hii itakufanya kutokuwa na mwendelezo kwasababu mwezi uliopita uliweke kiasi kikubwa utaona mwezi huu hutaweka. bila kiwango kilichowekwa, akiba hubaki kama wazo tu. Hivyo basi kama unataka kuwa mwaminifu katika kuweka akiba panga kiasi ambacho utakoweza kila mwezi bila kuharibu bajeti yako.
Suluhisho: amua asilimia ndogo ya kipato (mfano 5–10%) ambayo utaweka akiba moja kwa moja kila mwezi, useweke akiba kubwa sana ambayo utakubana katika mpango wako wa kila mwezi, weka akiba ambayo ukiiweka haitaathiri bajeti yako ya kila mwezi.
Kubadilisha tabia hizi hakuhitaji kuwa tajiri; kunahitaji uamuzi mdogo wa kila siku na kukumbuka kwa nini ulianzisha safari ya “hatua kwa hatua”.
Hitimisho
Mara nyingi tunataka kubadilisha maisha yetu ya kifedha bila kugusa tabia ndogo za kila siku zinazoonekana hazina madhara. Ukweli ni kwamba, tabia hizo ndogo zikijumlishwa kwa miezi na miaka zinakuwa mzigo mkubwa kwenye kipato chetu. Ukianza kuzitambua na kubadilisha moja baada ya nyingine kuandika matumizi, kuepuka ununuzi wa haraka, kupunguza mikopo ya starehe utagundua mabadiliko makubwa bila hata kuongeza kipato chako. Chagua tabia moja uibadilishe wiki hii, kisha ongeza nyingine baadaye.
Maoni
Chapisha Maoni